Thursday, August 25, 2016

UMUHIMU WA WANAWAKE KWA KANISA (Nguvu ya Waombaji)




“Lakini lisikieni neno la BWANA, enyi wanawake, Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake; Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila mmoja jirani yake kulia. Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu, imeingia majumbani mwetu; Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje, na vijana katika njia kuu. Nena, BWANA asema hivi, Mizoga ya watu itaanguka kama samadi juu ya mashamba, Na kama konzi ya ngano nyuma yake avunaye, wala hapana mtu atakayeikusanya” (Yeremia 9:20-22)

Mara nyingi watu hawajui kwamba MAMBO yanayotokea MADHABAHUNI ni majibu ya MAOMBI ya “watu wa Mungu”, waliyoomba kwa dhati huko FARAGHANI, na sasa Bwana anatenda mbele ya macho ya kila mtu, hadharani.

Nabii Yeremia anasema, kuna mauti imeingia ndani kupitia dirishani; vijana wanaangamia huko nje, na kwenye njia kuu, lakini dawa haipo huko nje, dawa ipo ndani kwa hawa WANAWAKE waombaji; tena imewapasa wawafundishe na binti zao, ili waombe mbele za Bwana juu ya nchi na watu wake, ili Bwana aokoe watu.

Fikiri wakati ule Bwana anakamatwa na watu wenye silaha, wanakwenda kumsulubisha. Petro na wenzake wako mbali kabisa wala hawataki kuhusika na hiyo shida, lakini Mariam, mama yake Bwana, akiwa na umri wa tarkiban miaka 60, pamoja na wale wanawake wengine wachache, wanamfuata Bwana hadi mwisho, bila kujali wabebao mikuki na upanga. Ndipo Bwana akiwa juu, ameangikwa msalabani tayari, anatazama chini, anamwona mama yake pale analia, anamwambia ,“Mama, tazama, mwanao” (Yohana 19:26b). Ukiangalia huyu mama, pamoja na umri wake kusogea, pamoja na kutembea kutoka mbali sana, akifuatilia kila kitu kwa karibu, yamkini alikesha na kushinda njaa siku kadhaa, huko nje anapigwa na baridi wakati wengine wanaota moto; hatimaye anamwona mwanaye wa kwanza, kifungua mimba wake, anapigiliwa misumari juu ya mti. Huyu mama akiwa hapo, anaona jinsi mwanae anachomwa mkuki ubavuni! Hebu fikiri Yusufu mume wake alikuwa wapi?


Sasa ndivyo ilivyo hata sasa. Wako wanawake huko kanisani, yamkini hawana hata kanga ya kubadili, wengine ni wajane. Wengine hawajui kula milo miwili, wakishindia uji, basi kesho tena ndio watakutana na bakuli nyingine na kipande cha mhogo mkavu. Lakini ni waaminifu katika maombi mbele za Bwana daima. Wapo kanisani, na Bwana anawajua. Huko mbele madhabahuni miujiza inafanyika, watu wanapona, watu wanachanga hela kama wamerukwa na akili, huku wakiyainua majina ya watumishi “hao” kama miungu. Wanawake hawa wako kimya kule nyuma, wamesimama katika nafasi zao kwa uaminifu tu, na Mungu anatenda.

Tazama, mwonekano wa “hao” watumishi, ni kama wafalme wakuu, ukipiga thamani ya mavazi yao, mikufu shingoni, viatu, nk., bei yake haifai kusema hadharani. Wanajisifu kwa mali zao, na kutaja vitu vikubwa walivyonavyo, ambavyo watu wengine hawana; fahari yao iko katika farasi, magari ya farasi na majumba ya kifalme. Kumbe kule nyuma yuko mwanamke mwombolezaji kasimama katika zamu yake; anakesha katika nafasi yake ya ulinzi, usiku na mchana, akimwomba Mungu afungue watu. Hakuna amjuaye wala kumjali, kwa maana kwa jinsi ya nje watu kama hawa hawana cha kuvutia. Ibada ikiisha, baadhi yao, utawaona wakiharakisha kituoni, wakiwahi daladala, wakati mwingine mvua inawanyeshea na huko nyumbani hawajui cha kula jioni. Ukisikia neno hili “watafutwa machozi”, usidhani kila mtu anaelewa maana yake, wapo watu ambao siku ile ya mwisho watang'aa kama nyota, na mataji makubwa sana ya utukufu yatakuwa vichwani mwao, KILA chozi litafutwa na Bwana mwenyewe. Wakati huo, wapo WENGI watakataliwa, haijalishi majina yao makubwa na miujiza mingi waliyosifiwa kwayo, kumbe! nyuma yao kulikuwa na waombelezaji (waombaji) ambao hawakujulikana na mtu, ila Bwana aliwajua. Kama unasimama katika nafasi hii, nakutia moyo, songa mbele kwa uaminifu, bado kitambo kidogo tu, Bwana anakuja kumlipa kila mtu sawa na matendo yake. Kila chozi lako lililodondoka ukiomba kwa ajili ya kanisa na huduma, litafutwa.

Ukifuatilia habari za kuzaliwa kwa Bwana, utaona Mariam na Yusufu wanapitia kipindi kigumu. Wakuu wa nchi, wafalme na wenye mamlaka, wanafanya vita kumwangamiza mtoto. Mariamu ni binti mdogo tu, sio tajiri na hana jina kuu, ila anajikuta kwenye vita na mfalme wa nchi, Herode na jeshi lake. Kumbe huku nyuma yuko mtu mwingine, asiyefahamika na mtu, jina lake ni Simion, anakesha na kuomba kwa ajili ya Bwana, hadi Bwana anazaliwa Simion anakesha katika kuomba. Simion akapata taarifa, akiongozwa na Roho Mtakatifu, akaenda Hekaluni kumwona mtoto na kumpakata mikononi mwake, na kumshukuru Mungu na kusema, “Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi” (Luka 2:29-35). Simeoni anamshukuru Mungu kwa kumaliza kazi yake, na sasa anaomba kibali cha KUPUMZIKA na watu wake (kufa).



Ukiangalia kitabu cha Tito 2:3-5 utaona Paulo anasema, “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe” (Tito 2:3-5). Hapa tunaona WAJIBU wa wanawake kufundisha wanawake wenzao, kwanza kwa MATENDO yao; pili, kuwafundisha kwa kuwaambia jinsi iwapasavyo kuenenda katika ndoa zao, nk. ILI “neno la Mungu lisitukanwe”. Huu ni wajibu mkubwa sana. Lengo hapa ni “Neno la Mungu lisitukanwe”. Hebu fikiri ni faida kubwa kiasi gani wanawake wakijua kujitunza, na kuenenda katika utakatifu na kuwa mfano wa kuigwa? Sisemi wanaume hawahusiki, ila ona jambo hili kwa msisitizo wake. Ukitaka kuona taifa linaangamia, nyima wanawake nafasi yao katika jamii, hii sio bibilia tu, hata katika mifumo ya kijamii. Wanawake ndio “mwili”, wanaume ni “vichwa” tu; kichwa bila mwili, hakuna kitu cha maana kitafanyika hapo.

Angalia wajibu wa wanawake kwa waume zao, “Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume” (Yeremia 31:22). Kuna WAWILI walioitwa “msaidizi”: kwanza, Hawa (mwanamke – msaidizi wa kufanana na Adam); na pili, Roho Mtakatifu (Msaidizi mwingine). Sasa kuna maeneo ambayo “mlinzi na msaidizi” (mwanamke) akilala kwenye ndoa yake, maisha yatakuwa magumu tu, sio kwa mume wake tu, bali kwa nyumba nzima. Kumbuka, ili mabinti wakae sawa, LAZIMA wafundishwe kwa matendo/mifano jinsi ya kuwa waombolezaji (waombaji na wacha Mungu), ama sivyo “mauti inaingilia madirishani na kuangamiza watu” (Yeremia 9:20-22). Ukiangalia nafasi nyingine ya kufundisha (role model), kusudi ni ili “Neno la Mungu lisitukanwe”. LAZIMA shule ianzie kwenye ngazi ya familia, huko kwenye ndoa (Tito 2:3-5). Sasa usisahau kwamba Kanisa linaanzia kwenye ngazi ya familia, huko kwenye familia kukikaa vibaya, huku kanisani kazi ya mchungaji ni ngumu.

Natamani kila mwanamke na kila mwombaji (walinzi wa Israel, wa kike na wakiume) waone jambo hili kwa undani, wavae silaha zao, na kuchukua nafasi zao katika ulimwengu wa roho.

No comments:

Post a Comment